.

Friday, March 19, 2010

SUGU ABURUZWA KWA PILATO..!!

Kesi hiyo iliyofunguliwa katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Dsm, ni kutokana na kauli ya msanii huyo kwamba kampeni iliyozinduliwa jijini Dar es Salaam, Februari 13 mwaka huu dhidi ya malaria, ilitokana na wazo lake.

Kesi hiyo iliyoko mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Joyce Minde, MNM wanawakilishwa mahakamani hapo na Kampuni ya Uwakili ya Excellent Attorney and Advocates ya jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka ya kesi hiyo, mlalamikaji ameieleza mahakama kuwa msanii huyo na washirika wake, Deiwaka Entertainment na William Mungai, hawana mamlaka na haki zozote za kisheria kwenye mradi huo.

Aidha, kabla ya kuanza kusikilizwa kwa kesi ya msingi, walalamikaji wamewasilisha ombi la awali la kutaka mahakama kumzuia Sugu kuitisha mkutano wowote na vyombo vya habari kuhusiana na suala hilo. Kesi hiyo itaanza kusikilizwa Machi 24, mwaka huu.

Hivi karibuni, Sugu alidai kuwa waandaaji wa kampeni hiyo ya ‘ZINDUKA Malaria Haikubaliki,’ iliyozinduliwa katika viwanja vya Leaders, Dar es Salaam na Rais Jakaya Kikwete, hawakumshirikisha, hivyo kuiba wazo lake.

Mradi huo unaolenga kutoa ujumbe wa kupambana na malaria, umekuwa na utata kuhusu nani alibuni wazo hilo, kwani Sugu anadai ni wazo lake la muda mrefu.

Taasisi ya MNM ni asasi ambayo imekuwa ikifanya kazi zake tangu mwaka 2006 ya kukomesha malaria barani Afrika na imekuwa ikishirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii tangu mwaka juzi ikisambaza vyandarua 267 katika kampeni ya taifa ya kukinga watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Kwa mujibu wa MNM, kampeni hiyo ilisifiwa kwa mafanikio ikiwa na lengo la kupeleka ujumbe kwa Watanzania kwamba malaria inaweza kukingwa na kutibiwa.

Sugu katika madai yake, alisema alitoa wazo la kushirikisha wasanii katika kampeni hiyo lakini wakati maandalizi yanafanywa hakuhusishwa hadi kupatikana kwa wasanii zaidi ya 20 walioshiriki.

MNM katika taarifa yake, ilisema mwaka juzi Mkurugenzi wake wa Mawasiliano, Martin Edlund, alikutana na Sugu kwa bahati ndani ya ndege wakiwa safarini kuja Tanzania.

“Martin alikuwa katika ziara ya utafiti wa kupata watu wazuri ambao wangeweza kusaidia katika kuandaa kampeni ya kitaifa dhidi ya malaria ... hatua kama hiyo ilishafanyika nchini Senegal kwa kushirikiana na mwanamuziki nguli, Youssou N’Dour,” ilisema taarifa.

Ilisema MNM awali ilitambulishwa kwa Kampuni ya matamasha nchini ya Round Trip, na mshirika wa kibiashara wa Sugu aitwaye William Mungai wa Kampuni ya Deiwaka Entertainment.

“Baada ya utafiti wa kina, Round Trip ilitambuliwa kama kampuni inayoweza kuitangaza na hata kuandaa uzinduzi wa kampeni hiyo na kusaini mkataba na MNM mwaka jana. “Si Sugu wala Mungai waliohusishwa katika mpango wa uzinduzi wa tamasha la ZINDUKA,” ilisema taarifa.

Iliongeza kuwa MNM pia ilifanya utafiti wa kupata wasanii waliopo nchini na kuamua kuwa itashirikiana na wasanii Profesa Jay, Bi Kidude, Lady Jaydee, Banana Zorro, THT, Mwasiti na Marlaw, ili kusambaza ujumbe wa kupambana na malaria nchini kama sehemu ya mkakati wa kufanikisha kampeni hiyo.

Ilisema MNM si asasi ya kutengeneza faida na imekuwa ikifanya kazi yake tangu mwaka 2006 ya kukomesha malaria barani Afrika na imekuwa ikishirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii tangu mwaka juzi, ikisambaza vyandarua 267 katika kampeni ya taifa ya kukinga watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

No comments:

Post a Comment

,